24/04/2026
Prison
HALI YA HATARI MAGEREZANI NORD-KIVU: WAFUNGWA 29 WAFARIKI KATIKA ROBO YA KWANZA YA 2026.
Nord-Kivu, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Hali ya magereza katika Mkoa wa Nord-Kivu imeelezwa kuwa ya kutisha kufuatia vifo vya Wafungwa 29 vilivyoripotiwa katika kipindi cha miezi mitatu ya kwanza ya mwaka 2026.
Kwa mujibu wa mtandao wa kutetea haki za binadamu wa Réseau pour les droits de l’homme (REDHO), vifo hivyo vimerekodiwa katika magereza mawili makuu ya eneo hilo, likiwemo Gereza la Kangbayi lililopo Beni na Gereza la Kakwangura lililopo Butembo.
Taarifa hiyo inaeleza kuwa, “jumla ya Wafungwa 29 wamepoteza maisha katika robo ya kwanza ya mwaka 2026,” huku ikibainisha kuwa Wafungwa 20 walifariki katika Gereza la Kangbayi Mjini Beni na wengine 9 katika Gereza la Kakwangura Mjini Butembo.
Sababu kuu zinazotajwa kuchangia vifo hivyo ni msongamano mkubwa wa Wafungwa, ukosefu wa lishe bora, pamoja na ucheleweshaji wa taratibu za kimahakama.
Kwa mujibu wa REDHO, “idadi kubwa ya Wafungwa wanazuiliwa bila hukumu kwa muda mrefu,” hali inayochangia kuongezeka kwa msongamano Magerezani.
Takwimu zinaonyesha kuwa zaidi ya Wafungwa 3,300 wanashikiliwa katika Magerezani hayo mawili kwa sasa, ambapo wengi wao wapo katika kizuizini cha muda bila kusikilizwa kesi zao Mahakamani.
Mashirika ya haki za binadamu yanatoa wito kwa mamlaka za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kuchukua hatua za haraka kuboresha hali ya Magerezani, kuharakisha mienendo ya kesi Mahakamani, na kuhakikisha haki za msingi za wafungwa zinalindwa.
Toa maoni yako